Msumbiji: Mkoa wa Zambezia

Rudi kwenye Utafiti

Mkoa wa Zambézia upo katikati mwa Msumbiji, ukipakana na Mkoa wa Tete na Mkoa Sofala upande wa Magharibi, Mkoa wa Niassa upande wa Kaskazini, mkoa wa Nampula upande wa Kaskazini-Mashariki na bahari ya Hindi upande wa Kusini. Zambézia ina jumla ya eneo la kilomita za mraba  105,000, ambalo ni takriban ukubwa wa nchi za Scotland na Wales kwa pamoja.

Zambézia ina msimu mmoja wa mvua kwa mwaka, tabia yake ya hali ya hewa, kulingana na uainishaji wa Köppen-Geiger, ni ya kitropiki ikiwa na eneo kubwa la savana ya kitropiki. Msimu wa mvua ni kati ya Novemba na Machi na wastan wa kiwango cha mvua ni 70 mm kwa mwezi; msimu wa kiangazi ni kati ya Aprili na Oktoba na kiwango cha mvua kwa wastani ni 12 mm kwa mwezi. Lakini, kuna mwenendo wa jumla wa kupungua kwa mvua ya msimu, kutokana na upungufu wa mvua mnamo Oktoba na Novemba. Upungufu wa siku za mvua za msimu hutokea hasa kati ya Februari-Aprili na upungufu ni mkubwa zaidi katika maeneo ya pwani na kaskazini mwa Zambézia. Matokeo yake, tabaka la uoto wa asili huathirika kwa kupungua na hali ni mbaya zaidi katika hatua za mwanzo za msimu. Zambézia ndio mkoa wenye joto zaidi nchini humo,kiwango cha chini cha joto hushuka hadi nyuzi 20 za Celsius na kiwango kikubwa cha joto ni kati ya nyuzi 30 hadi 35 za Celsius kwa mwaka mzima.

Chanzo: E. Gevorgyan / ZALF

Udongo ni fluvisols katika maeneo ya pwani, lakini pia kuna acrisols na ferralsols katika nyanda za juu. Kwa muktadha huu, mkoa wa Zambézia unaweza kuwekwa katika maeneo makuu manne ya ikolojia ya kilimo:

  1. Ukanda wa pwani na ukanda mdogo wa pwani,
  2. Kanda za kati (za (2a) Zambezia na (2b) Niassa),
  3. Kanda za juu na
  4. (upande wa magharibi) eneo la bonde la mito ya Zambezi na Chire

Mazao makuu yanayozalishwa kwenye eneo linalo limika katika mkoa huo ni mihogo, mahindi, viazi vitamu, mazao ya jamii ya mikunde (k.m. Kunde na mbaazi) na – katika ukanda wa pwani na ukanda mdogo wa pwani – mchele. Karibu mazao yote yanazalishwa kwa kilimo cha kutegemea mvua.

Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2017, Zambézia ina wakazi milioni 5.1, moja ya mikoa yenye watu wengi nchini Msumbiji. Kiutawala, mkoa umegawanywa katika wilaya 16 tofauti, ikiwemo wilaya ya Gúruè – eneo ambalo Vegi-Leg inatekelezwa. Gúruè ina eneo la jumla ya kilomita za mraba 5600 na 6% ya watu (takriban 420.000) wanaishi katika wilaya hii.

Vegi-Leg mahsusi inafanya kazi katika maeneo mawili madogo ya kiutawala, Lioma na Mepuagiua, ambapo ndani yake kuna kijiji cha Ruace na mji wa Nicoropale. Kulingana na hesabu rasmi ya idadi ya watu, Ruace ina wakazi 5.625 sawa na kaya 1.125 na wakazi wa Nikoropale ni 46.272 sawa na kaya 10.616. Katika maeneo yote haya mawili, wakulima wengi wanajihusisha na kilimo kidogokidogo na mazao makuu yanayozalishwa ni mahindi, mtama, mihogo, ufuta, tumbaku, aina mbali mbali za maharagwe, soya, karanga, chai na mazao anuwai ya bustani.

Ramani ya vijiji vya Mradi katika Mkoa wa Zambezia